Habari

​Wakuu wa Vyuo vya FDC wakutana Shirika la Elimu Kibaha


Shirika la Elimu Kibaha (KEC) leo Ijumaa tarehe 10/03/2023 limekuwa mwenyeji wa kikao kazi cha wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kanda ya Mashariki kilichofanyika katika Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC).

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Anathe Nnko, amewakaribisha wakuu hao wa vyuo na kuwataka kujadili utekelezaji wa shughuli zao kwa kuzingatia kuboresha utoaji wa huduma bora ya elimu.

“Tunawashukuru kwa kuchagua chuo chetu kuwa mwenyeji wa kikao chenu. Karibuni sana. Vyuo vya maendeleo ya wananchi ni tofauti na vyuo vingine kwa kuwa vinawawezesha wananchi kupata ujuzi wa aina mbalimbali kwa vitendo zaidi ili kuwasaidia kujiajiri. Naamini kwenye kikao hiki mtabadilishana uzoefu ili kuhakikisha mnajiimarisha zaidi katika elimu mnayoitoa,” amesema Bw. Nnko.

Kikao kazi hicho cha siku moja kimehudhuriwa na wakuu wa vyuo vya FDC kutoka Wilaya za Kilosa, Kibaha, Malinyi, Rufiji, Kisarawe, Kilombero na Morogoro mjini kwa lengo la wakuu hao kubadilishana uzoefu na kupanga masuala ya pamoja yanayohusiana na uendeshaji wa vyuo wanavyovisimamia.