Habari

Walimu Kituo cha Malezi na Makuzi ya Watoto-Tumbi wapongezwa


Walimu wa Kituo cha Malezi na Makuzi ya Watoto- Tumbi kilichopo chini ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) wamepongezwa kwa kuwafundisha vyema na kuwawezesha wanafunzi wake kuelewa kwa usahihi mahiri zote tatu yaani Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Elimu, Shirika la Elimu Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya tatu ya kituo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bertil Mellin na kuhudhuriwa na baadhi ya watumishi wa Shirika la ELimu Kibaha (KEC) pamoja na wazazi wa watoto 85 waliohitimu elimu ya awali.

Dkt. Shemwelekwa amesema walimu wa Kituo cha Malezi na Makuzi ya Watoto-Tumbi wanafanya kazi kubwa kuwafundisha watoto nidhamu mbali ya kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.

“Wazazi, nawaomba mtoe ushirikiano kwa walimu kwa sababu wanawajenga kuwa na utambuzi pamoja na kuwa na nidhamu,” amesema Dkt. Shemwelekwa.

Katika hatua nyingine, wazazi wamefurahishwa jinsi watoto walivyojengewa uwezo wa utambuzi wa masomo pamoja na nidhamu.

Katika mahafali hayo, watoto waliwaonesha wazazi jinsi wanavyosoma irabu, kuimba na kufanya maigizo ambayo yaliwavutia wazazi pamoja na wegeni mbalimbali akiwemo mgeni rasmi, Dkt. Shemwelekwa.

Baada ya maonesho hayo, watoto hao walisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Dkt. Shemwelekwa na kumshukuru Mungu kwa kuwapatia walimu bora na kuwafudisha mahiri zote tatu yaani Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.