Habari

​Walimu Shirika la Elimu Kibaha wapongezwa kwa kufaulisha mitihani ya Taifa, 2022


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Robert Shilingi, leo Jumanne tarehe 07/02/2023 amewapongeza watumishi walimu na wasio walimu wa shule za msingi na sekondari zilizopo chini ya Shirika la Elimu Kibaha kwa kuwezesha matokeo mazuri ya mitihani ya kitaifa iliyofanyika mwaka 2022.

Bw. Shilingi amezitoa pongezi hizo kwenye mkutano wa wafanyakazi wa Shirika la Elimu Kibaha kwa kuwazawadia vyeti na fedha taslimu watumishi walimu ambao wanafunzi wao wamefaulu kwa asilimia 96 katika mitihani ya taifa iliyofanyika mwaka 2022, na watumishi wasio walimu waliochangia katika mafanikio ya kurugenzi ya huduma za elimu iliyopo kwenye Shirika hilo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Bw. Shilingi ameeleza kuwa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) limeendelea kitekeleza majukumu yake muhimu ya kupambana na adui ujinga, maradhi na umasikini kwa njia ya kutoa elimu. Na pia ametoa pongezi kwa watumishi hao kufanikisha kufikia malengo ya Shirika.

"Kwa namna ya pekee niwapongeze walimu na watumishi wote wasio walimu kwa matokeo mazuri ya mitihani ya kitaifa katika shule zetu zote za msingi na sekondari. Aidha, kwa nafasi ya pekee, nitoe pongezi kwa uongozi wa shule ya sekondari Kibaha kwa kufaulisha wanafunzi wote 91 wa kidato cha nne 2022 kupata daraja la kwanza," alisema Bw. Shilingi.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa kurugenzi ya huduma za elimu, Dkt. Rogers Shemwelekwa amewataka watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kujenga taasisi bora na kuwezesha Shirika la Elimu Kibaha kutekeleza vyema majukumu yake.

Tuzo hizo zimetolewa kwa walimu 15 ambao ni Filbert Kisomvu, Festo Swisbert, Deodart Joseph, Mango Kondo, Viarney Kilapilo, Hamisi Chiza, Mariam Msuya na Julius Ngasa kutoka shule ya sekondari Kibaha; Richard Mswahili, Rosemary Mwenda na Hajirati Abdulnul kutoka shule ya sekondari ya wasichana Kibaha; Zefania Malindila, Maulid Mputa na Eric Namadengwa kutoka shule ya sekondari Tumbi; na Consolata Komba kutoka shule ya msingi Tumbi.

Watumishi wasio walimu waliopatiwa tuzo kwa kuisaidia kurugenzi ya huduma za elimu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ni Geofrey Kisonga - msimamizi wa miradi, Andrew Mbala - dereva, Baraka Hamza - muhasibu, Mussa Mwanga na Paskali Msopole watumishi wa maktaba.