Habari
Walimu Shirika la Elimu Kibaha watakiwa kujiunga CWT
Walimu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) wametakiwa kujiunga na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ili kuipa CWT nguvu ya kutetea maslahi mbalimbali ya walimu nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa tarehe 22/04/2022 na Katibu Mkuu wa CWT, Bw. Deus Seif wakati akizungumza na walimu wa Shirika la Elimu Kibaha kujibu changamoto zao kuhusu utekelezaji wa mwongozo wa 2010, waraka mpya alioutoa Katibu Mkuu wa utumishi ambao unaanza Julai mwaka huu na maslahi ya walimu waliokaa kwenye cheo kimoja kwa muda mrefu.
Katika kikao hicho, Bw. Seif amewasisitiza walimu wa KEC ambao hawajajiunga na CWT kujiunga na chama hicho kwa kuwa watapata nguvu ya kutetea maslahi yao pamoja na changamoto mbalimbali.
“Sisi kama chama cha CWT msingi wetu ni kuwatetea wanachama wetu, tafadhali tuungane, tusitawanyike, tusidharau muungano wetu, tuungane pamoja,” amesisitiza Bw. Seif.
Bw. Seif amesema CWT kwa muda mrefu imekuwa ikitetea maslahi ya walimu wote wakiwemo wale ambao hawajajiunga na chama hicho.
Akizungumzia maslahi hayo, Katibu Mkuu huyo amesema kwamba waliokaamuda mrefu bila kupandishwa madaraja watapewa madaraja ya mserereko kunzia Julai 01, 2022.
Amefafanua kwamba walimu ambao wapo kwenye ajira, mishahara yao haitashushwa bali watabaki na mishahara walionayo, lakini hawatapandishwa viwango vya mishahara mpaka kiwango chao kifikie kwenye waraka mpya.
“Suala ambalo linakwenda kutekelezekaka hivi karibuni ni upandishaji wa vyeo kwa mserereko,”amefafanua Bw. Seif.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha, Bi. Devotha Shija amemuomba Katibu Mkuu wa CWT kufuatilia kwa karibu suala la muundo ili walimu waweze kunufaika.
Kikao hicho kiliudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Robert Shilingi, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, wakuu wa shule za msingi, sekondari na vyuo, walimu, wajumbe wa CWT Taifa, Mkoa wa Pwani na wilaya zake.