Habari

Wanafunzi KEC wapata mafunzo namna ya kuanzisha biashara


Wanafunzi wa shule za sekondari zilizopo chini ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) leo Alhamisi tarehe 20/04/2023 wamepata fursa ya kujifunza namna ya kuanzisha biashara na kuziendeleza.

Mafunzo hayo wamepatiwa na wanafunzi wenzao wa Shule ya Sekondari ya Thoren iliyopo Orebro nchini Sweden ikiwa ni sehemu ya ziara yao katika Shirika hilo.

Wanafunzi hao wameonyesha mfumo wa utoaji wa elimu unaotumika katika Shule yao ambako somo la ujasiriamali ni lazima kusomwa na wanafunzi wote katika kipindi chote wanachosoma elimu yao ya sekondari.

Elimu hiyo ya ujasiriamali ilihusu namna ya kutafuta wazo la biashara, sababu za kuanzisha biashara husika na mchango wa biashara hiyo kwa jamii, kuchagua jina la biashara na kutengeneza alama ya biashara.

Pia, wanafunzi wa Shirika walipatiwa elimu namna ya kuunda uongozi wa biashara husika kwa nafasi mbalimbali, namna ya kutambua wateja na kutafuta masoko na kuweka utaratibu wa kuhakikisha biashara husika inaendelea kukua zaidi.

Fursa ya utoaji wa elimu hiyo ya ujasiriamali kutoka kwa wanafunzi Shule ya Sekondari Thoren kwenda kwa wanafunzi wa shule za sekondai Kibaha, Tumbi na Kibaha wasichana zilizopo chini ya Shirika la Elimu Kibaha ni moja ya faida ya urafiki uliopo kati ya Shirika la Elimu Kibaha na nchi ya Sweden.