Habari

​Wanafunzi Sekondari ya Wasichana Kibaha waibuka washindi utafiti wa upungufu wa maji Mto Ruvu


Wanafunzi wawili wa kidato cha tatu, Gloria Benatus Tibaijuka na Halima Said Muhunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha leo Jumanne tarehe 13/12/2022 wamekabidhi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Bw. Robert Shilingi zawadi walizopokea baada ya kuibuka washindi wa jumla katika shindano la wanasayansi chipukizi la kuibua matatizo na kutafuta suluhu ya matatizo hayo kwenye jamii inayowazunguka.

Akizungumza baada ya kukabidhi zawadi hizo, Gloria Tibaijuka ametoa shukurani kwa Mungu, walimu na wazazi kwa ushirikiano waliowapa mpaka kutimiza ndoto zao za kushinda shindano hilo. Na ameeleza kuwa utafiti wao ulihusu kutambua tatizo la upungufu wa upatikanaji wa maji katika chanzo cha maji cha Mto Ruvu ambao unasambaza maji kwenye mikoa mitatu ya Pwani, Dar es Salaam na baadhi ya sehemu za mkoa wa Morogoro wakilenga kutafuta suluhisho la tatizo hilo.

“Utafiti wetu ulijikita kwenye upatikaji wa maji, matumizi ya maji hayo ya Mto Ruvu kwa binadamu, mifugo, viwanda, kilimo, na utunzaji wa mazingira ya chanzo hicho cha maji kwa miaka 14 mfululizo kuanzia mwaka 2011 hadi 2025. Baada ya utafiti huo, tuligundua kuwa uzalishaji wa maji Mto Ruvu ni mdogo kuliko mahitaji ya mikoa inayohudumiwa na chanzo hicho na uharibifu wa mazingira yanayozunguka mto Ruvu ni mkubwa kuliko uhifadhi wake.

“Hivyo tumependekeza uhifadhi wa mazingira ya Mto Ruvu uboreshwe kikamilifu kwa kuzuia uharibifu kama vile ukataji miti, uingizaji wa mifugo, kulima pembezoni mwa mto na vitafutwe vyanzo vingine vya maji kwa ajili ya kuongeza wingi wa maji ya kuhudumia mikoa hiyo mitatu kama vile kuchimba visima vya maji, kuvuna maji ya mvua na kusafisha maji ya bahari ili yatumike kwa mahitaji ya binadamu,” amesema Gloria.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Robert Shilingi amewapongeza wanafunzi hao kwa ushindi walioupata kwani umeleta sifa kwao wenyewe, shule yao na Shirika kwa ujumla.

“Gloria na Halima wametuthibitishia kuwa watoto wa kike wanaweza kufanya mambo makubwa sana. Tafiti waliyoifanya imelenga kujibu changamoto zilizopo kwenye jamii. Huku ni kuunga mkono juhudi za Serikali yetu ya awamu sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani yeye mwenyewe anatuonyesha mfano mzuri kuwa wanawake wanaweza kwa mambo makubwa anayoifanyia nchi yetu. Nawapongeza sana wanafunzi hawa na kuhamasisha wanafunzi wetu wengine kufanya tafiti nyingi zaidi maana uwezo wanao na Shirika litawasimamia kutimiza ndoto zao,” amesema Bw. Shilingi.

Naye, Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la Young Scientist Tanzania kwa Mkoa wa Pwani, Bw. Paul Balibate ameeleza kuwa, shirika hilo liliendesha mashindano hayo kuanzia mwezi wa tatu mwaka huu na jumla ya tafiti 1187 ziliwasilishwa, kati ya hizo tafiti 380 zilionekana kukidhi vigezo na kushindanishwa kitaifa. Baada ya kushindanishwa shule ya Sekondari ya wasichana Kibaha, tafiti yake ikaibuka mshindi wa jumla kitaifa kati ya tafiti hizo 380 zilizoshindanishwa.

Pia, Mkurugenzi wa Huduma za Elimu wa Shirika la Elimu Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa amewapongeza wanafunzi hao kwa utafiti waliofanya kwani umelenga kutatua changamoto za jamii na utafiti huo unazidi kuonyesha mchango wa Shirika la Elimu Kibaha katika maendeleo ya nchi yetu.

“Nafarijika sana kuona Shirika la Elimu Kibaha tunaendelea kuwa kinara. Uwekezaji wa Serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye elimu matunda yake yanaonekana. Nawapongeza sana wanafunzi hawa kwa kutumia ujuzi walionao kwa maendeleo ya taifa letu,” amesema Dkt. Shemwelekwa.

Matokeo ya mashindano hayo yalitolewa rasmi Serena Hotel tarehe 08/12/2022 na Shirika la Young Scientist Tanzania na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha walipewa fedha taslimu Shilingi 1,500,000, vikombe vitatu, medali mbili na udhamini wa masomo ya elimu ya juu ‘university scholarship’ na taasisi ya Karimjee Foundation. Pia wamepata nafasi ya kwenda kuwasilisha utafiti wao Afrika Kusini na Ireland.

Utafiti ni moja ya shughuli za Shirika la elimu Kibaha ukiwa na lengo la kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla kupitia elimu.