Habari

WANAFUNZI WA SHULE ZA SEKONDARI ZA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KULETA MABADILIKO KATIKA UJASIRIAMALI KWA JAMII


WANAFUNZI WA SHULE ZA SEKONDARI  ZA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KULETA MABADILIKO KATIKA UJASIRIAMALI KWA JAMII

Tarehe: 28 Septemba ,2017

Wanafunzi wa Shule za Sekondari za Shirika la Elimu Kibaha wanatarajiwa kuleta mabadiliko katika ujasiriamali kwa jamii hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Robert Shilingi wakati akizindua rasmi ushirikiano baina ya Shirika la Elimu Kibaha na Chuo cha Biashara cha  Thoren kutoka nchni Sweeden.

Bw. Robert Shilingi amebainisha kuwa Chuo cha Biashara cha Thoren kimeingia rasmi katika mashirikiano na Shirika La Elimu Kibaha  ambapo wanafunzi wa Shule zote za Sekondari za Shirikia  watapatiwa elimu ya ujasirimali na biashara ili wamalizapo masomo waweze kuwa chachu ya kuelimisha jamii na hao wenyewe kushiriki kikamilifu  katika ujasiriamali.

Kwa upande wake Mratibu wa Mashirikiano hayo kutoka Sweden Bi. Sirpa Rydell amesema Kuwa Chuo chake kimeingia katika mashirikiano na Shule za Shirika la Elimu Kibaha ili kuwajengea uwezo wa elimu na mbinu mbalimbali za ujasiriamali ili kuwawezesha wamalizapo masomo waweze kujiajiri na kujitegemea.

Akielezea namna mradi huo utawanufaisha wanafunzi Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu Bw. Chrisdom Ambilikile amesema mashirikiano hayo yanalenga kuwapa uwezo wanafunzi elimu ya ujasiriamali na kutoa elimu kwa  jamii mzima inayoizunguka  Shirika kuhusu biashara na  namna ya kujiajiri.

Mapema Mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Elimu Kibaha Mwalimu Mchayano Ngonyani amesema mradi unalenga kushiriki pamoja  na juhudi za Serikali za kutengeneza ajira. Alibainisha Nchini Tanzania ajira nyingi zinategemewa kupatikana Serikalini huku nafasi hizo bado ni chache hivyo elimu ya ujasiriamali inaweza kuwa chachu ya kuwapatia ajira vijana wanaohitimu shule kwa kufanya biashara.

Shirika la Elimu Kibaha lilianzishwa mwaka 963 wakati huo ikijulikana kama Tanganyika Nordic Project na baadaye mwaka 1970 Mradi huo ukakabidhiwa rasmi kwa Tanzania na kuwa Shirika la Elimu Kibaha.