Habari
Watahiniwa 155 waahidi kuongoza kitaifa matokeo kidato cha sita 2022
Mahafali ya 55 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Kibaha yamefanyika jana Alhamisi tarehe 05/05/2022 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, huku wanafunzi watahiniwa wakiahidi kuongoza kitaifa kwenye matokeo ya mitihani yao.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi wa mahafali hayo, mmoja wa wanafunzi wahitimu wa kidato cha sita Bw. Carlos Mwita, ameeleza kuwa Shule ya sekondari Kibaha imeendeleza ufaulu mzuri kitaaluma kwa kidato cha nne na cha sita katika mitihani ya taifa licha ya changamoto mbalimbali.
“Kwa kipindi cha mwaka 1997 mpaka 2020, shule yetu imekuwa kati ya shule kumi bora kitaifa katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita. Hata hivyo mwaka huu tunadhamiria kufanya vizuri katika mitihani yetu, kupata wote daraja la kwanza na kuwa katika shule tatu bora za kwanza zitakazofanya vizuri kitaifa.”Amesema Bw. Mwita.
“Tuna upungufu wa walimu wa somo la kompyuta pamoja na mafundi sanifu wa maabara; uhaba wa vifaa vya michezo; uhaba wa vifaa vya chumba cha kompyuta; na upungufu wa matenki ya maji na pampu ya kusukuma maji.”
Akimwakilisha mgeni rasmi wa mahafali hayo Meneja wa benki ya CRDB Kanda ya Mashariki Bw. Badru Iddi, Bi. Rose Kazimoto ambaye ni Meneja wa benki ya CRDB tawi la Kibaha amewataka wanafunzi wahitimu wa kidato cha sita kwa mwaka huu 2022, kuongeza kasi ya kutafuta elimu bora ili kuweza kushinda kwenye ushindani wa soko la ajira.
“Muongeze kasi ya kujituma ili mpate elimu bora na siyo bora elimu itakayowasaidia kutimiza ndoto na malengo mliyojiwekea katika maisha kwa kuwa dunia ya sasa ni ya ushindani mkubwa, hivyo usipoipata elimu bora na kuifanyia kazi unapunguza nafasi yako ya ushindani katika soko la ajira.”
“Shule hii ni ya wanafunzi wa vipaji maalum, imeleta sifa kubwa sana katika mkoa wetu wa Pwani kwa kuwa na ufaulu wa hali ya juu na pia kwa kushika nafasi ya kwanza mara kwa mara katika Mkoa.”
“Napenda kuwakumbusha vijana wetu mnaohitimu leo kuwa bado safari yenu ya kimasomo inaendelea na imani yangu kuwa mwaka huu wote mtafaulu katika daraja la kwanza kama mlivyoahidi.” Amesema Bi. Rose.
Aidha Bi. Rose amewata uongozi wa Shule ya Sekondari Kibaha kuwasilisha CRDB maombi rasmi ya kusaidiwa kutatua changamoto walizoziwasilisha kwa kuwa CRDB wana utaratibu wa kutoa asilimia moja ya faida wanayoipata kila mwaka na kuirudisha kwa jamii katika sekta za elimu, afya na mazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha, Bw. Jonasi Mtangi amemshukuru mgeni rasmi kwa kufika katika mahafali hayo na kueleza kuwa tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 1965 mpaka sasa imetoa wahitimu zaidi ya elfu kumi na mbili, na wanafunzi wanaohitimu sasa idadi yao ni 155.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Robert Shilingi amewatakia kila la kheri watahiniwa wote wa kidato cha sita na ameahidi kuwapa zawadi maalum watahiniwa wote 155 iwapo watafanya vizuri na shule ya Sekondari Kibaha itaingia kwenye shule tatu bora zitakazofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita ya mwaka huu.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Robert Shilingi, wakuu wa shule na vyuo vilivyopo Shirika la Elimu Kibaha, wajumbe wa bodi ya shule; walimu na wafanyakazi wasio walimu wa shule ya sekondari Kibaha, mwenyekiti wa kamati ya wazazi; wazazi, walezi na wanafunzi