Habari

​Watoto 85 wahitimu mafunzo ya awali Shirika la Elimu Kibaha


Mahafali ya pili ya Kituo cha Watoto Wadogo Tumbi yamefanyika leo Alhamisi tarehe 01/12/2022 katika Ukumbi wa Bertil Mellin Kibaha ambapo jumla ya watoto 85 wamehitimu.

Akisoma taarifa ya kituo hicho, Mwalimu Mkuu wa kituo hicho, Bi. Martha Anania amesema kituo chao kinalenga kulea na kutoa msingi bora wa elimu kwa watoto.

“Kituo chetu kina uwezo wa kulea watoto zaidi ya 131 na kimekuwa kikitoa watoto bora kila mwaka wanaojiunga na elimu ya msingi kutokana na walimu bora tulionao na wanaofanya kazi kwa bidii,”alisema Bi. Anania.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa mahafali hayo, ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma za Elimu katika Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Dkt. Rogers Shemwelekwa amewapongeza walimu na wazazi wa watoto wahitimu kwa malezi na kuwataka wazazi kuwaendeleza zaidi kielimu watoto wao.

“Falsafa ya Hayati Mwalimu Nyerere kuanzisha Shirika la Elimu Kibaha ni kupambana na maadui watatu wa maendeleo ambao ni ujinga, umasikini na maradhi. Hivyo kwa ninyi kuwaleta watoto wenu katika kituo hiki niwahakikishie kuwa mmefanya maamuzi sahihi,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

“Safari ya kumsomesha mtoto na kumuandaa kufanya vizuri ni ndefu sana, wazazi tuendelee kushirikiana na walimu ili watoto wetu wajengwe kwenye misingi mizuri. Huu ni uwekezaji mnaoufanya wazazi kwa watoto wenu ili waje kuwa kizazi kizuri kwa maendeleo yao binafsi, jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

Watoto hao wahitimu, walitumia siku yao ya mahafali kuonesha mbele ya mgeni rasmi na wazazi wao baadhi ya masomo waliyokuwa wakijifunza. Kituo cha watoto wadogo Tumbi, ni sehemu bora ya kulea na kufundisha watoto na hupokea watoto wapya kila mwaka wenye umri kuanzia miaka mitatu hadi mitano.