Habari

​Watumishi Shirika la Elimu Kibaha (KEC) washiriki maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani


Watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) leo tarehe 01/05/2022 wameshiriki maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) ambayo kimkoa yamefanyika Wilaya ya Mkuranga katika viwanja vya shule ya msingi Juhudi.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Aboubakar Kunenge ambaye amewataka watumishi kutimiza vyema majukumu yao.

"Mhe. Rais wetu mwezi January mwaka huu alieleza vipaumbele vyake nane kimoja wapo ni kudumisha demokrasia,utawala bora na utawala wa sheria, hivyo mliopewa mamlaka ya kusimamia taasisi zenu, timizeni wajibu wenu katika kusimamia maslahi ya watumishi." Amesema Mhe. Kunenge.

"Tujitume tubadilishe Mkoa wetu na maisha yetu. Tumedhamiria kubadilisha Mkoa wetu uwe Mkoa bora zaidi." Amesema Mhe. Kunenge.

Pia Mhe. Kunenge amewataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kutoa ushirikiano ili kufanikisha matukio ya Sensa na anuani za makazi, pia kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa virusi vya UVIKO-19.

Katika maadhimisho hayo, Mhe. Kunenge aliweza kutoa zawadi na vyeti vya pongezi kwa wafanyakazi hodari kutoka katika taasisi, mashirika na Halmashauri zilizopo kwenye Mkoa wa Pwani.

Aidha maadhimisho haya kitaifa yamefanyika katika Mkoa wa Dodoma ambapo mgeni rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Rais amewahakikishia watumishi kuwa nyongeza ya mshahara kwa watumishi ipo kuanzia mwezi Julai, 2022.

"Ulezi wa mama unaendelea, lile jambo letu lipo, siyo kwa kiwango kilichosemwa na TUCTA, kwa sababu hali ya uchumi wa nchi yetu na uchumi wa dunia siyo nzuri sana, uchumi wetu ulishuka mno tumejitahidi sana kuupandisha na kwa sababu tulishatoa ahadi mwaka jana, nimeagiza jambo liwepo, mahesabu yanaendelea tutajua lipo kwa kiasi gani lakini jambo lipo." Amesema Mhe. Samia.

Kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi kwa mwaka huu 2022 ni 'Mishahara na Maslahi Bora kwa Wafanyakazi ndio Kilio chetu: Kazi Iendelee'.