Habari

​Watumishi wa KEC wapewa elimu kuhusu huduma za PSSSF


Watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) leo Jumanne tarehe 06/09/2022 wamepewa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ikiwemo huduma ya mafao kwa watumishi wa umma.

Akitoa elimu hiyo, Afisa Matekelezo Mwandamizi wa PSSSF Mkoa wa Pwani, Bw. Deogratias Njuu amewataka watumishi wa KEC kuelewa michango yao kwenye mfuko wa PSSSF na namna wanavyoweza kunufaika na mfuko huo.

"Wajibu wa mwanachama wa PSSSF ni kuhakikisha michango yako ipo salama. Unaweza kuona michango yako kwa simu kupitia 'application' inayoitwa PSSSF kiganjani mwako." Alisema Bw. Njuu.

Bw. Njuu ameeleza kuwa watumishi wenye vigezo vya kupata mafao ni wale waliochangia kwenye mfuko kwa miezi 180 na kuendelea.

"Kwa watumishi ambao wamechangia kwenye mfuko wa PSSSF kwa miezi 180 na kuendelea, wana nafasi ya kulipwa mafao mbalimbali yanayotolewa na mfuko yakiwemo mafao ya kustaafu, uzazi, ulemavu na ugonjwa," alisema Bw. Njuu.

Watumishi wa KEC walielezwa kuwa Mwezi Juni, 2022 Serikali imebadili kikokotoo cha mafao ambapo watumishi watalipwa kwa kufuata mfumo wa asilimia 33 kwa mafao ya mkupuo na asilimia 67 kwa pensheni ya kila mwezi. Na iwapo mstaafu akifariki dunia wategemezi wake watalipwa pensheni yake ya miaka mitatu kwa mkupuo.

Elimu hiyo ililenga kujenga uelewa wa watumishi wa KEC juu ya mabadiliko ya kikotoo, usajili wa wanachama, uwasilishaji wa michango, mafao na masuala ya madai