Habari

Watumishi wastaafu 23 waagwa Shirika la Elimu Kibaha


Watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha leo Ijumaa tarehe 21/10/2022 wamefanya sherehe ya kuwaaga watumishi wastaafu 23 wa Shirika hilo ikiwa ni ishara ya kuonyesha upendo kwao na kuthamini ushirikiano walioutoa kipindi wakiwa wafanyakazi wa Shirika hilo.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, mwenyekiti wa kamati ya kuwaaga wastaafu Bi. Hellen Swai amewatakia wastaafu hao kila la kheri kwenye maisha yao baada ya utumishi na kuwashukuru kwa kuutumikia umma kwa uaminifu na uadilifu.

"Sisi tunaoendelea na Utumishi wa umma, tunawatakia maisha mema wastaafu wetu, tutaendelea kutumia ujuzi mliotuachia hadi muda wetu wa kustaafu utakapowadia kwa mujibu wa sheria." Amesema Bi.Swai.

Pia kwa niaba ya wastaafu walioagwa leo, Bw. Alexander Kashaija ametumia sherehe hiyo kuwaasa watumishi wanaoendelea na utumishi wa umma kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa wabunifu.

"Uaminifu, uadilifu, weledi na kujiendeleza kielimu ni vitu vya kuvizingatia sana katika kuimarisha utendaji kazi wenu." Amesema Bw. Kashaija

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Anathe Nnko amewapongeza wastaafu hao na kuwataka kudumisha ushirikiano waliokuwa nao kwenye jamii wanayoishi nayo.

"Kila mmoja kati yenu ana mchango wake katika mafanikio ya Shirika hili, tunathamini sana michango yenu, mmeacha alama nzuri, na tutaendelea kutumia uzoefu wenu."

"Katika maisha baada ya utumishi, muendelee kutunza afya zenu, kujiwekea ratibu ya kufanya shughuli nyingine za jamii ili kuendelea kuimarisha miili na akili zenu. Karibuni sana Shirika la Elimu Kibaha, sisi ni familia moja tuendelee kushirikiana." Amesema Bw. Nnko.

Sherehe hiyo ya kuwaaga wastaafu 23 wa Shirika la Elimu Kibaha imefanyika katika ukumbi wa Bertil Mellin uliopo katika Shirika hilo.