Habari

Zainabu Vulu: Ukatili wa kijinsia haukubaliki


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Pwani, Bi. Zainabu Vulu leo amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha kusoma kwa bidii, kujilinda na kuhakikisha hawarubuniwi ili waweze kutimiza ndoto zao kupitia elimu wanayoipata.

Bi. Zainabu Vulu amezungumza hayo leo Jumamosi tarehe 29/04/2023 akiwa katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha ambayo ipo chini ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) akiwa mgeni rasmi kwenye mbio za hisani zilizoanzishwa na kikundi cha kijamii cha wanawake kinachojulikana kwa jina la ‘Women Marathon’ kwa lengo la kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia na kutoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi hao.

“Hakikisheni mnasoma kwa bidii masomo yenu ya shule. Ili mtimize ndoto zenu, muwe wasikivu kwa walimu na wazazi, msome kwa bidii kwa maendeleo yenu binafsi na familia zenu.

“Mnapaswa kujikinga na ukatili unaofanywa huko nje, muwe na ushirikiano mzuri na walimu wenu, msiogope kusema, kuweni huru ili mpate kusaidiwa. Kuna msemo unayojulikana kwa jina la don’t touch, muutumie kuhakikisha hakuna mtu anayekurubuni na kuuchezea mwili wako, jilindeni mtimize ndoto zenu” amesema Bi. Zainabu Vulu.

Katika mbio hizo za hisani wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha wamepata fursa ya kupatiwa taulo za kike (pedi) 500 na kupewa elimu ya jinsia kutoka kwa wadau mbalimbali wa kikundi cha kijamii cha ‘Women Marathon’, Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) na dawati la jinsia mahala pa kazi kutoka Shirika la Elimu Kibaha.

Akiwashukuru wadau hao, Farida Masenga, kiongozi mkuu wa wanafunzi na mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha amesema elimu waliyopatiwa kuhusu namna ya kupinga ukatili wa kijinsia itawasaidia kuwa wajasiri katika kusimamia haki zao na taulo za kike walizopatiwa zitawasaidia kusoma kwa utulivu hasa kipindi wakiwa katika hedhi.