Habari

Zao la alizeti lawanufaisha wanafunzi Kibaha


Wanafunzi wanaosoma mchepuo wa kilimo katika Shule ya Sekondari Kibaha na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC) wananufaika na kilimo cha alizeti katika shamba lililopo Shirika la Elimu Kibaha (KEC).

Kauli hiyo, imetolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Bw. Anathe Nnko baada ya kutembelea shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 35 ili kukagua maendeleo ya zao hilo.

Bw. Nnko amesema wanafunzi hao wamenufaika na kilimo cha alizeti kupitia wataalamu wa kilimo ambao wamewawezesha kupata ujuzi na maarifa ya kuanzisha kilimo cha zao hilo.

“Lengo kubwa ni kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuhusu kilimo cha alizeti pamoja na shughuli za ufugaji,” amesema Bw. Nnko.

Amesema zaidi ya wanafunzi 800 wa Shule ya Sekondari Kibaha na wanafunzi zaidi ya 300 wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC) wamenufaika na mafunzo ya zao la alizeti.

Afisa Kilimo wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Sikitu Mwakyeja amesema kilimo cha alizeti kinaongeza kipato kwa ajili ya shirika kwa kuuza mafuta na mashudu.

Bw. Mwakyeja amesema wanatumia mbegu aina ya chotara HYSUN 33 ambayo ina uwezo wa kutoa kilo 800 hadi 1000 za mbegu za alizeti kwa ekari moja.

“Mwaka jana tulipata lita 1200 baada ya kuvuna kilo 3,530 za alizeti na mashudu kilo 1,518 baada ya kulima ekari 20,” amesema Bw. Mwakyeja.

Amesema kwamba kilimo cha alizeti ni kizuri kwa kuwa zao hilo lina soko kubwa katika jamii kwa sababu baada ya mavuno yanapatikana mafuta na mashudu ambayo yanaingiza kipato.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Bw. Anathe Nnko, amesema Shirika linatarajia kuanza utafiti wa mazao ya mizizi ikiwemo mihogo na viazi vitamu kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti cha TARI Kibaha lengo kubwa likiwa ni kuwawezesha wanafunzi kupata elimu kwa vitendo kuhusu kilimo cha mazao hayo.

Bw. Nnko amesema utafiti unatarajia kuanza mwishoni mwa mwaka huu na baada ya utafiti kukamilika, matokeo ya utafiti yatawanufaisha wanafunzi na jamii kwa kuwa ni wadau wa shughuli za kilimo.

“Kupitia utafiti huu, wanafunzi wetu watajifunza mambo mengi kuhusu kilimo cha mazao ya mizizi na watajifunza njia bora za kulima viazi na mihogo,” amesema Bw. Nnko.

Mbali na Shirika la Elimu Kibaha kusimamia shule za sekondari, msingi na vyuo pia linaendesha shughuli za kilimo, ufugaji wa nyuki na ng’ombe wa maziwa.