Habari

CHUO KIKUU CHA MOUNT KENYA WAONESHA NIA KUJENGA CHUO KIKUU SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA


Chuo kikuu cha Mount Kenya kinatarajia kufanya uwekezaji katika eneo la Shirika la Elimu Kibaha (SEK) ,hayo yamesemwa na Mbunge wa Kibaha Mjini Mhe.  Silvester Koka wakati akiwatambulisha Mmiliki na Mhadhiri wa Chuo Kikuu  hicho kwa Menejimenti ya Shirika la Elimu Kibaha leo katika ukumbi wa mikutano wa Shirika.

Akitambulisha Chuo hicho Mhe. Koka amesema Chuo kina uzoefu mkubwa katika Elimu ya Chuo  Kikuu kwani wana mtandao mkubwa wa Chuo hicho katika nchi za Afrika Mashariki ikwemo Uganda ,Rwanda na pia Somalia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Elimu Kibaha akiutambulisha ugeni huo amesema kuwa SEK ni Taasisi ya  Elimu iliyoanzishwa miaka 50 iliyopita kwa ajili ya kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga ,maradhi na umasikini.

Alifafanua kuwa Hayati Mwalimu Nyerere kwa kutambua maadui  hao na kutumia  ushirikiano na Nchi za Skandinavia aliamua Shirika hili lianzishwe kupambana na  maadui hao.

Aidha amesema Shirika limejikita katika kutoa huduma kwa wananchi kupitia Sekta ya Elimu ambapo kuna  Shule kuanzia Chekechea hadi Sekondari, Sekta nyingine ni Afya hapo  kuna Hospitali ya Rufaa ya Tumbi na Chuo cha Utabibu na kwamba ili kufanikisha azma ya kupambana na umasikini kuna Sekta ya Huduma za jamii  kuna Chuo cha KFDC ambapo watu mbalimbali hupata mafunzo ya ufundi na stadi mbalimbali na  wakulima hupata mafunzo ya kuongeza ubora katika uzalishaji.

Pia Dk. Mpemba amesema Shirika lina ardhi kubwa yenye zaidi ya heka 3000 kwa ajili ya uwekezaji ambapo tayari wawekezaji wawili wamekwisha anza kuwekeza ambao ni Organia watakaojega kiwanda cha kisasa cha uzalishaji wa  kuku na Watumishi Housing watakaojenga nyumba kwa ajili ya Watumishi wa Serikali.

Kwa upande wake Mmiliki wa Chuo cha Mount Kenya Dk. Simon Kichage amesema anatambua katika ulimwengu wa sasa Taasisi za Serikali na Binafsi huungana kwa pamoja katika kuleta maendeleo yaani (Public Private Partnership) na ndio maana wamekuja Shirika la Elimu Kibaha ili kuona ni jinsi gani wanaweza kushirikiana na SEK katika sekta ya Chuo Kikuu kwa kuzingatia Shirika la Elimu Kibaha lina ardhi kubwa kwa ajili ya uwekezaji.

Serikali imekuwa ikihimiza kila Taasisi ijitahidi kupanga mikakati ya kuongeza mapato ya ndani na uwekezaji katika sekta mbalimbali ni moja ya juhudi hizo.