Habari
DR ZAINAB CHAULA ATOA SOMO NAMNA BORA YA KUONGEZA MAPATO YA HOSPITALI YA TUMBI
DR ZAINAB CHAULA ATOA SOMO NAMNA BORA YA KUONGEZA MAPATO YA HOSPITALI YA TUMBI
Tarehe 7 Oktoba 2016,
Naibu Katibu Mkuu Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Zainabu Chaula ametoa somo namna bora ya kuongeza mapato ya Hospitali ya Tumbi na kuongeza ufanisi katka utoaji huduma za afya. Dr Chaula ameyasema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Hospitali ya Tumbi leo katika Ukumbi wa B.Merlin.
Aidha,Dkt. Chaula ambaye hivi karibuni ameteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Naibu Katibu Mkuu Afya Tamisemi , amesema anatambua changamoto zilizopo katika hospitali nyingi nchini na kwamba changamoto hizo zinaweza kutatuliwa kwa ushirikiano wa pamoja. Amewataka watumishi wa Sekta ya Afya kushirikiana kwa pamoja kutatua changamoto hizo kwa kupanga mipango na kuwa wabunifu katika kuongeza mapato ya Hospitali ambayo yakiongezeka yataweza kutatua changamoto nyingi za hospitali ikizingatiwa changamoto hizo zinatatuliwa na rasilimali fedha.
Awali akielezea mafanikio na changamaoto zinazoikabili Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi Dkt Bryceson Kiwelu amesema kuwa Hospitali ya Tumbi ni Hospitali ambayo kwa sasa ina sifa nzuri ya kuhudumia majeruhi wanaopata ajali za barbarani hususan barabara ya Morogoro na maeneo jirani na kwamba wengi wa majeruhi hutibiwa kwa misamaha kiasi kinachosababisha hospitali kukosa fedha za kununulia dawa.
Ametaja changamoto nyingine ni ukosefu wa damu salama kwa ajili ya kuhudumia majeruhi .miundo mbinu ya hospitali kuhitaji marekebisho makubwa,na deni kubwa la dawa na vifaa tiba ambapo MSD na wazabuni wengine wanadai zaidi ya Sh milioni 700.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bi Chiku Wahady alimshukuru Naibu Katibu Mkuu Afya Dr Zainab Chaula kwa kuongea na watumshi wa Hospitali ya Tumbi na kwamba ushauri wote wa namna ya kuongeza mapato na kuboresha huduma utafanyiwa kazi ili changamoto zilizopo ziweze kutatuliwa. Hospitali Teule ya Rufaaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi ilipata hadhi hiyo mwaka 2011.