Habari
HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA PWANI TUMBI YAPEWA SIFA KATIKA UTOAJI WA HUDUMA
- SHERIA IMETAKIWA KUCHUKUA MKONDO WAKE KWA WAHUSIKA KATIKA UKATILI WA KIJINSIA
TAREHE 17/10/2018
Na: Lucy Semindu SEK - Kibaha
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameitaka jamii kutofumbia macho wahalifu wote wa ukatili wa kijinsia kwa kuwafikisha kwenye mkondo wa sheria ili kumaliza ukatili nchini.
Ameyasema hayo wakati akikagua kituo cha cha huduma ya kudhibiti ukatili wa jinsia (one stop center) cha mkoa wa Pwani kilichopo Tumbi hospitali alipofanya ziara ya siku moja alisema kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia nchini kwa watoto na wanawake.
Alionya jamii kutomalizana wao wenyewe bali wawapeleke wahalifu kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake na kuhakikisha haki inatendeka kwa waathirika wa matukio hayo ya ukatili wa kijinsia.
Pia aliwaonya wauguzi na madaktari nchini wasikubali kurubuniwa na waalifu wa makosa hayo kwa kuharibu ushahidi na iwapo wakibainika kufanya kosa hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni zao.
Aidha aliwataka wahanga wa matukio ya ukatili wa kijinsia kuwahi mapema kwenye vituo vya kuthibiti ukatili wa jinsia wahudumiwe haraka sambamba na sheria kuchukua mkondo wake.
Hata hivyo Naibu waziri huyo alitembelea na kukagua mapokezi ya wagonjwa katika hospitali ya mkoa ya Tumbi, wodi ya akinamama na watoto, kitengo cha damu salama, stoo ya dawa ya hospitali hiyo, maabara, ikiwa ni pamoja na kukagua ujenzi wa upanuzi wa jengo jipya la hospitali ya Tumbi.
Aidha Dkt. Ndugulile aliwataka wafamasia wote nchini kutoa taarifa ya kila wiki kuhusu kiasi cha dawa na aina ya dawa zilizopo hospitalini ili mgonjwa ahudumiwe kwa ufasaha kulingana na aina za dawa zilizopo.
“wafamasia watoe taarifa kila wiki ya aina ya dawa na idadi ya dawa zilizopo stoo husika ili kuepusha mgonjwa kuandikiwa dawa ambazo hazipo kwenye stoo ya hospitali husika na kusababisha usumbufu kwa mgonjwa”
Dkt. Ndugulile amepongeza huduma mbalimbali bora zinazotolewa katika hospitali ya Tumbi. Amewataka watoa huduma ya afya waendelee kuboresha huduma hizo ili kuongeza zaidi ubora wa huduma hospitalini hapo.
Lakini pia alitoa tuzo mbali mbali kwa vituo vya afya na zahanati za mkoa wa Pwani zilizofanya vizuri wakati wa ukaguzi wa ubora wa utoaji huduma wa zahanati na vituo vya afya mkoa wa Pwani ambapo zahanati tano zilipata tuzo.