Habari

HOSPITALI YA TUMBI YAPOKEA MSAADA WA VIFAA TIBA


HOSPITALI YA TUMBI YAPOKEA MSAADA WA VIFAA TIBA

  • NI KUTOKA SHIRIKA LA LIFE MINISTRY

Na : Lucy Semindu – 19/05/2017

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi imepokea msaada wa vifaa tiba kutoka Shirika la kidini la Life Ministry. Shirika hilo limetoa msaada wa  vifaa tiba  vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni ishirini.

Akipokea vifaa hivyo Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya wa Shirika la Elimu kibaha ambaye pia ndiye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Tumbi Dkt. Edward Wayi amesema msaada huo wa vifaa tiba umepokelewa wakati muafaka ikizingatiwa  Hospitali ya Tumbi inapokea majeruhi wengi wanaotokana na ajali za barabarani .

Amemshukuru Mkurugenzi wa Life Minstry Mchungaji Dismas Shekalaghe kwa Shirika lake kuweza kujitoa kusaidia kuokoa maisha ya binadamu. Dkt. Wayi ameeleza msaada huo utasaidia Hospitali kutoa huduma bora zaidi na kwamba changamoto kubwa  inayoikabili Hospitali ya Tumbi ni dawa   na vifaa Tiba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Life Ministry Mchungaji Dismas Shekalaghe amesema kuwa Shirika lake lilianza rasmi mwaka 1985 hapa Tanzania na toka kipindi hicho wamekuwa wakijuhusisha na masuala ya kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa visima virefu na huduma nyinginezo,

Amebainisha kwamba  mwaka huu wamejikita katika kutoa huduma ya vifaa Tiba kwenye Hospitali zenye uhitaji mkubwa wa vifaa tiba na kwamba wanatambua Hospitali ya Tumbi inapokea majeruhi wengi na pia hutoa huduma bora  ndiyo maana wameamua Hospitali ya Tumbi iwe ni Hospitali ya kwanza nchini Tanzania kupata vifaa tiba kupitia Shirika hilo la Life Ministry.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi ni Hospitali ambayo inaendelea kupokea majeruhi wa ajali za barabarani na mahitaji ya vifaa tiba bado ni makubwa sana.