Habari

Siku ya Wanawake Duniani Machi, 2017


SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA

HOTUBA YA MAADHIMISHO YA SIKU WANAWAKE DUNIANI SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA TAREHE 8/3/2017

Habari za asubuhi ‘Wanawake wote’ na wageni waalikwa wote mlioshiriki nasi katika Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.

Awali ya yote tunamshuruku Mungu kwa kutuwezesha kufikia siku hii ya leo. Ni furaha ya pekee kujumuika kwa pamoja na wanawake wa Shirika la Elimu Kibaha, katika kuadhimisha siku hii ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.

Kama ilivyo ada siku hii huadhimishwa kila mwaka Machi 8. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tanzania ya Viwanda: Wanawake ni Msingi wa Mabadiko kiuchumi”.

Ikumbukwe kuwa, wanawake ndio washauri pamoja na watendaji wakuu katika familia na Taifa kwa ujumla. Mchango wa mwananmke katika kujenga nchi ni mkubwa kwani, mwanamke ana ushawishi mkubwa katika kuhamasisha vijana (watoto) kuanzia malezi bora, kusoma kwa bidii na kufanya kazi kwa bidii.

Shirika la Elimu Kibaha kama Taasisi ya Umma ina jumla ya watumishi 818 kati ya hao watumishi takribani 400 ni wanawake. Kwa takwimu hizo ni dhahiri kuwa, nafasi ya wanawake katika maendeleo ya Shirika la Elimu Kibaha na Taifa kwa ujumla ni mkubwa na kwamba, Serikali ya Tanzania inatupa kipaumbele katika ajira na tunashukuru kwa hilo.

Mbali na kushirikishwa katika masuala ya kimaendeleo, wanawake wa Shirika la Elimu Kibaha wamekuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi sehemu zao za kazi hii inapelekea kushuka kwa ufanisi wa kazi zao za kila siku. Changamoto nyingine ni kupungua kwa ushirikiano kati yetu, ambao unasababisha utengano mfano kutoshiriki katika shughuli za kijamii kwa wingi kama vile sherehe na misiba. Inafikia wakati unakuta watu wanaoshiriki ni wale tu walio karibu. Tunaomba wanawake tuwe chachu ya ushirikiano na upendo wetu kama watoto wa baba mmoja ili turudishe ushirikiano na upendo tuliokuwa nao sehemu ya kazi na hata tuwapo nje ya Shirika la Elimu Kibaha.

Hitimisho, tunapenda kumshukuru Mwajiri wetu kwa kutupa kibali cha kushiriki/kuadhimisha siku hii muhimu ya wanawake Duniani ndani ya Shirika la Elimu Kibaha na pia tunawashukuru wanawake na baadhi ya wanaume wa Shirika na nje ya Shirika kwa kuchangia fedha ambazo zimetumika kununulia zawadi mbalimbali kwa ajili ya watoto waliolazwa katika wodi ya watoto katika Hospitali yetu ya Tumbi. Pia tunawashukuru wale wote waliojitolea damu katika Kitengo cha Damu Salama Tumbi Hospitali zoezi ambalo lilianza tarehe 1/3/2017 na litamalizika 10/3/2017.

Mwisho kabisa tunapenda kuwakumbukusha waandaji wa sherehe hizi za siku ya Wanawake Duniani katika ngazi ya Wilaya na Mkoa kufanya maandalizi mapema ikiwa ni pamoja na kutoa barua za mialiko mapema ili na sisi wanawake wa Shirika la Elimu Kibaha tuweze kushiriki nao. Mwaka huu 2017 Shirika limechelewa kupata mwaliko toka ngazi za Wilaya ndio maana tumeamua kusherehekea katika maeneo ya Shirika la Elimu Kibaha.

Wanawake wa Shirika la Elimu Kibaha oyeeeeeeee!!!! Ahsante sana.

Imeandaliwa na Kamati ya Maandalizi ya

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani