Habari
Kilele cha Mahafali ya 57 Shule ya Sekondari Kibaha
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Anathe Nnko leo tarehe 12/10/2023 amewataka wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Taifa ya kumaliza kidato cha nne ambayo itaanza tarehe 13/11/2023 hadi 30/11/2023 kuendelea kujiandaa ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.
“Nawatakia mitihani mema, mkijiamini mtafanya vizuri, endeleeni kujiandaa vizuri,” amesema Bw. Nnko.
Katika hatua nyingine, Bw. Nnko amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bw. James Mbalwe kwa kutoa msaada wa kisima cha kuhifadhia maji lita laki moja na matenki matano ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita elfu kumi kila moja kwa ajili ya huduma ya maji kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha.
Katika mahafali hayo, pia, Bw. Nnko amewashukuru walimu wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa kuwa na malengo makubwa ya kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika mitihani mbalimbali.
Mgeni rasmi katika mahafali ya 57 ya kidato cha nne yaliyofanyika katika Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, Bw. James Mbalwe amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufikia malengo yao.
Pia, Bw. Mbalwe amewataka wanafunzi hao waendelee kuwa na nidhamu kwakuwa nidhamu ni msingi wa mafanikio.
Naye, Mwenyekiti wa Wazazi Shule ya Sekondari Kibaha, Prof. Anthony Sangeda amewaomba wazazi waendelee kuwaombea wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne ili waweze kutimiza malengo yao.
“Wanangu moto ni single digit (daraja la kwanza lenye tarakimu moja) Mungu awasaidie kama moto wetu unavyosema. Wazazi muendelee kuwaombea watoto wetu ili watimize malengo yao. Kwa vijana wa kidato cha nne tunawaombea, tunaomba muendelee kupambana kama ambavyo mmeahidi, tunawatakia heri watoto, muendelee kushikamana, muwe kitu kimoja na tupo pamoja nanyi,” amesema Prof. Sangeda.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Elimu, Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Fidelis Haule amewashukuru walimu wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo pamoja na wazazi kwa kuweza kujitolea kwa hali na mali ili kuwezesha mafanikio shuleni.
Bw. Haule amemshukuru mgeni rasmi, Bw. James B. Mbalwe kwa kutoa msaada wa upatikanaji maji ya kutosha katika shule hiyo kwani mkono utoao ndio mkono upokeao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwanalugali, Bw. Shomari Mguta amewashukuru walimu kwa malezi bora kwa wanafunzi wa Shule hiyo, lakini pia amefurahishwa na wanafunzi kuwa na nidhamu nzuri kwa jamii inayoizunguka Shirika la Elimu Kibaha.
Makamu Kaka Mkuu Mstaafu, Gration Sangeda akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake, amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kwa kutoa msaada wa kisima na matenki ya maji wenye jumla ya Shilingi 64,656,520. Pia wamewashukuru walimu na wafanyakazi wote wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa kuwawezesha kufika hapo walipo.