Habari

MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA KIKE WILAYA YA KIBAHA YAFANA • Yafanyika katika Shule yaSekondari ya Wasichana Kibaha Tarehe: 11/10/2018 Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Wilaya ya Kibaha yamefanyika leo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha


MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA KIKE WILAYA YA KIBAHA YAFANA

·   Yafanyika katika Shule yaSekondari ya Wasichana Kibaha

Tarehe: 11/10/2018

Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike Wilaya ya Kibaha yamefanyika leo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Assumpta Mshama ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha Bi. Sozy Ngate.

Bi Sozy Ngate amechukua muda wake mwingi katika hotuba yake kuwaasa watoto wa kike kutumia fursa waliyopata ya kusoma kwa bidii huku wakiweka malengo ambayo wanataka kuyafikia wamalizapo masomo.

Akisisitiza kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema imarisha uwezo wa mototo wa kike tokomeza ukeketaji,mimba na ndoa za utotoni ameitaka jamii kutoa ushirikiano wa kutosha ili kukabiliana na unyanyasaji wa watoto wanapobakwa, kukeketwa na kuepuka ndoa za utotoni.

Amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha  imekuwa ikifanya kazi bega kwa bega na OCD lakini wazazi hawatoi ushirikiano kwani humalizana na wahalifu kinyemela bila kufuata mkondo wa sheria.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Robert Shilingi amesema Taasisi yake imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu anayostahili na ndiyo maana wameweka mikakati ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya Shule ya Sekondari ya wasichana Kibaha.

Ametoa wito kwa jamii kijitokeza kwa wingi wakati wa harambee hiyo inayotarajiwa kufanyika mwezi wa Novemba huku Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Tulia Atickson kuunga mkono juhudi hizo.

Sherehe hizo zilipambwa na Ngojera,Nyimbo , Midahalo na Maigizo yote yakielekeza mapambano ya unyanyasaji wa mtoto wa kike na kutokomeza ukeketaji na mimba za utotoni kwani zinakwamisha ndoto ya maendeleo ya mtoto wa kike. Ambapo washiriki walitoka Shule ya Sekondari Kibaha, Shule ya Sekondari Tumbi, Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha na Shule ya Msingi Tumbi.

Katika risala yao Wanafunzi wameishukuru Serikali kwa kutoa elimu bure hivyo ni fursa kubwa kwao hasa kwa mtoto wa kike kuweza kujiendeleza na kufikia malengo waliyotarajia.

Naye mwanafunzi aliyewahi kusoma katika Shule ya Sekonadari ya Wasichana Kibaha ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Mwaka wa tano wa masomo ya udaktari katika Hospitali ya Bugando Bi Jacqueline Swai , amesema yeye wakati anasoma aliweka malengo na sasa ameyafikia. Amwataka wanafunzi wasidanganyike bali wasome kwa bidii na kufikia kila mmoja lengo alilojiwekea.

Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha ni miongoni mwa Shule za Shirika la Elimu Kibaha ikiwa na pamoja na Sekondari ya Kibaha ambayo imekuwa ya Kwanza kitaifa katika mitihani ya kidato cha sita kwa mwaka 2018 na Shule ya Sekondari Tumbi ambayo pia inafanya vizuri kitaaluma kiwilaya na kitaifa pia.