Habari

Mahafali kidato cha Sita yafana Kibaha Sekondari


Leo Alhamisi tarehe 27/04/2023 yamefanyika mahafali ya kidato cha sita ambapo jumla ya wanafunzi 183 wanatarajiwa kuanza mitihani ya kumaliza kidato cha sita mapema wiki ijayo.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa shule ya sekondari Kibaha Bw. George Kazi amesema kuwa malengo ya shule hiyo ni wanafunzi wote kufaulu kwa alama za juu.

"Malengo yetu ni kupata ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi wote wanaohitimu kidato cha nne na cha sita. Mwaka jana 2022 tulikuwa na wanafunzi 91 wa kidato cha nne, na wote walipata daraja la kwanza kuanzia pointi saba hadi kumi na moja".

Mgeni rasmi katika mahafali hayo Bw. Steven Kauzemi, meneja wa elimu kwa mlipa kodi, akimwakilisha Kamishna wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) amewapongeza wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari Kibaha kwa kufanya vizuri katika mambo mbalimbali ya kitaaluma na kuwatakia kila la kheri katika mtihani wao wa Taifa.

"Nawapongeza kwa matokeo mazuri mliyoyapata katika fani mbalimbali mnazozifanya. Naimani mtafanya vizuri katika mitihani yenu ya mwisho. Mizizi ya elimu ni michungu lakini matunda yake ni matamu."

"Naupongeza pia uongozi wa shule kwa kutambua umuhimu wa kodi katika nchi yetu hata kuanzisha klabu ya kodi kwa wanafunzi wenu. Hongereni sana na natoa wito kwa wanafunzi wahitimu kuwa mabalozi wazuri huko muendako". Amesema Bw. Steven Kauzemi.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa bodi ya shule Bw. Julius Manyerere, amemshukuru mgeni rasmi kwa kukubali kuhudhuria mahafali hayo, na ameahidi wanafunzi wa kidato cha sita kufanya vizuri katika mitihani yao.

"Tunakushukuru kwa kukubali mwaliko wetu, mbele yako wapo vijana 183 wanaohitimu kidato cha sita, vijana hawa wameandaliwa vizuri kitaaluma na tuna imani watapata matokeo mazuri katika mtihani wao wa Taifa". Amesema Bw. Manyerere.

Shule ya Sekondari Kibaha ilianzishwa mwaka 1965 ikiwa chini ya Shirika la Elimu Kibaha kwa lengo la kupambana na adui ujinga. Ni shule inayopokea wanafunzi wa vipaji maalum kutoka katika Halmashauri zote Tanzania.