Habari

Msajili wa Hazina alipongeza Shirika kwa ubunifu wa miradi ya maendeleo


Shirika la Elimu Kibaha (KEC) limepongezwa kwa ubunifu wa kuanzisha mradi wa Mafunzo ya Kukuza Ujuzi kwa njia ya Mtandao (SDF)) pamoja na kuandaa andiko la uanzishwaji wa shule ya msingi mchepuo wa kingereza na mafunzo ya ufundi.

Msajili wa Hazina Bw. Mgonya Benedicto alitoa pongezi hizo wakati alipokuwa akipokea taarifa ya miradi mbalimbali ya Shirika hilo.

Bw. Benedicto amesema Shirika hilo lina miradi mizuri ambayo inatekelezeka na kwamba KEC inapaswa kuangalia mbinu bora ya kuwafikia Watanzania wengi zaidi kupitia miradi wanayotarajiwa kuanzishwa.

“Nawapongeza kwa ubunifu wa uanzishaji wa miradi mipya, yote ni muzuri na nitaipitia na baadaye nitatoa maoni,” amesema Bw. Benedicto.

Awali, akiwasilisha taarifa ya miradi ya KEC, Meneja Uzalishaji Mifugo na Mazao wa Shirika hilo, Bw. Damas Msaki amesema Shirika lina miradi tisa ambayo inatarajiwa kutekelezwa baada ya kukamilika kwa taratibu za kuanzisha miradi hiyo.

Akizungumzia mradi wa Mafunzo ya Kukuza Ujuzi kwa njia ya Mtandao (SDF), Bw. Msaki amesema SDF ni moja ya miradi ya KEC ambayo umewavutia Watanzania wengi kusoma kupitia njia ya mtandao na kwamba Watanzania 6,541 wanasoma bure baada ya mafunzo kutangazwa.

“Hivi sasa Shirika linatoa mafunzo ya upishi, ushonaji, ufugaji kuku kibiashara, kilimo na bustani, ufundi magari, useremala, udereva, ufundi bomba na ufundi umeme wa majumbani kupitia njia ya mtandao.Tuna wanaume 3,583 sawa na asilimia 54 na wanawake 2,958 sawa na asilimia 45 ambao wanasoma mafunzo hayo,” amefafanua Bw. Msaki.

Bw. Msaki amesema miradi mengine inayotarajiwa kuanzishwa ni mradi wa mtaa wa viwanda wa ujasiriamali na ujuzi, mradi wa kuhuhisha shamba la ng’ombe wa maziwa na uanzishwaji wa bustani ya wanyama pori kwa ajili ya utoaji wa mafunzo ya uhifadhi.

Miradi mingine ni ukarabati wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCHOAS), ukarabati wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC), uanzishwaji wa shamba la mboga mboga kwa kutumia banda kitalu (Horticultural Greenhouse) na utoaji wa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vinavyonufaika na mikopo ili kuwawezesha kurejesha mikopo kwa wakati.

Bw. Msaki amesema miradi hiyo italiwezesha Shirika kuongeza wigo wa shughuli zake na kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

Msajili wa Hazina, ametembelea Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCHOAS) na ukarabati wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC).