Habari
SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KUANZA KUTUMIA MFUMO WA USIMAMIZI WA FEDHA- EPICOR JULAI- 2015
Kibaha- 4 Februari, 2015
Shirika la Elimu Kibaha linatarajia kuanza kutumia mfumo wa usimamizi wa fedha ( Epicor) ifikapo Julai ,2015. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Elimu Kibaha Dk. Cyprian Mpemba wakati akiwasilisha maada katika semina ya kujenga uelewa kuhusu mfumo wa epicor kwa menejimenti na wahasibu iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Shirika.
Aidha Dk. Mpemba amesema kuwa wakati umefika wa kukubali kubadilika na kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa na Serikali. Alibainisha kuwa mfumo huu utaweka nidhamu katika matumizi na usimamizi wa fedha kwa kuzingatia bajeti iliyopangwa.
Kwa upande wake Mwezeshaji toka TAMISEMI bwana Jeremia Mtawa amesema mfumo huu wa kiuhasibu utawezesha taarifa kupatikana kwa haraka zaidi huku ikiongeza uwazi na uwajibikaji. Alifafanua kuwa mfumo huu unaotumia teknolojia ya kisasa utaweza kuratibiwa TAMISEMI kwani kifaa maalum (server) kitawezesha kumbukumbu zote kusomeka huko.
Naye Meneja wa Tehama SEK bwana Annen Kimambo aliwasilisha maada kuhusu namna mfumo unavyofanya kazi. Aliishukuru TAMISEMI kwa msaada wa kifaa maalum cha kuwezesha kutunza kumbukumbu (server) na kutoa leseni itakoyowezesha Shirika la Elimu Kibaha kutumia kifaa hicho kwa ajili ya shughuli za kiuhasibu.
Mfumo wa Epicor unaotumika nchi nzima kwenye Halmashauri zote na Taasisi za Serikali kwa ajili ya shughuli za kiuhasibu na usimamizi wa fedha umeonesha mafanikio makubwa.