Habari
WATALAAM WA DAMU SALAMA WA MKOA WA PWANI WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI ZA UTOAJI HUDUMA YA DAMU SALAMA

WATALAAM WA DAMU SALAMA WA MKOA WA PWANI WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI ZA UTOAJI HUDUMA YA DAMU SALAMA
Na: Lucy Semindu – Kibaha
Watalaam wa damu salama wa Mkoa wa Pwani wametakiwa kuzingatia kanuni za utoaji huduma ya damu salama. Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt. Ruminius Kawili wakati akifungua mafunzo ya watoaji huduma ya damu salama wa Mkoa wa Pwani yaliyofanyika jana katika ukumbi wa jengo jipya la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi Kibaha.
Dkt. Kawili amesema kuwa damu salama ni muhimu sana katika kuokoa maisha ya watu hivyo ni muhimu kanuni zote zifuatwe ili damu atakayopatiwa mgonjwa iwe salama . Aliwaasa wawe wabunifu katika kazi yao kwa kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka ili watu wakubali kwa hiari kuchangia damu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa damu salama Kanda ya Mashariki Dkt. Evelyn Mgassa amesema kuwa katika suala zima la huduma ya damu salama bajeti ni kitu muhimu itakayowezesha shughuli zisikwame pia amesema damu ikusanywe kwa wachangia damu wa hiari na kwamba ubora na usalama wa damu uzingatiwe kwa kuhakikisha damu inapimwa kubaini ubora wake kabla hajapatiwa mgonjwa.
Aliwataka wataalam hao kutumia mafunzo watakayopata katika kuhakikisha kuna upatikanaji wa damu katika hospitali za wilaya wanazotoka, Alisisitiza kuwa itakuwa ni jambo la kushangaza mgonjwa anapewa rufaa katika hospitali nyingine kwa ajili ya ukosefu wa damu. Amewataka wahakikishe mgonjwa pale alipo apatiwe damu.
Naye mratibu wa damu Salama Kanda ya Mashariki Bw. N Towo amesema damu salama ni suala nyeti hivyo viwango vya ubora wa damu salama vinatakiwa kuzingatiwa .Damu salama ni muhimu kwa uhai wa mwanadamu hivyo huduma ya damu salama inatakiwa kuwa endelevu kwa kuhakikisha damu inapatikana pale inapohitajika.