Habari

Shirika la Elimu Kibaha laanzisha mafunzo ya Ujuzi na Ujasiriamali kwa njia ya mtandao


Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kupitia Chuo chake cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC) limetangaza kuanzisha mafunzo bure ya ujuzi na ujasiriamali kwa Watanzania kupitia njia ya mtandao.

Mafunzo hayo yanatolewa na Shirika hilo kwa ufadhili wa mradi wa kuendeleza ujuzi (SDF) wenye thamani ya Shilingi milioni 131 na unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 11/08/2022, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Robert Shilingi amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa miezi mitatu na yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 29/08/2022.

Mkurugenzi huyo amesema mafunzo ambayo yatatolewa kwa wananchi ni upishi, ufundi bomba, ushonaji, udereva, ufundi magari, ufundi uashi, useremala, ufundi umeme wa majumbani, ufugaji kuku kibiashara, kilimo na bustani, uchomeleaji, kompyuta na ujasiriamali.

“Lengo la mafunzo haya ni kuwapatia Watanzania elimu ya ujuzi ambayo itawajengea uwezo wa kujiajiri na baadaye kuwaajiri wenzao kupitia shughuli zao za ujasiriamali,” amesema Bw. Shilingi.

Bw. Shilingi amesema watu wenye uhitaji wa mafunzo hayo wanapaswa kujisajili kwenye mtandao ili wawaweze kupata nafasi ya kusoma.

“Namna ya kuomba kujiunga na mafunzo haya ni kwamba anayehitaji anapaswa kufungua www./https://elms.kec.or.tz na baada ya hatua hii, muhitaji atajaza fomu ya maombi na kuiwasilisha,” amefafanua Bw. Shilingi.

Mkurugenzi huyo amesema wahitimu watatunukiwa vyeti baada ya kumaliza mafunzo hayo ikiwa ni uthibitisho kwamba wamefuzu.

Naye, Mratibu wa Mafunzo ya Ujuzi na Ujasiriamali, Dkt. Rogers Shemwelekwa amesema kwamba mafunzo hayo yameanzishwa ili kuwawezesha Watanzania ambao wanapenda kusoma, lakini hawana fedha za kusoma mafunzo kama hayo.

“Tutakuwa na mafunzo ya nadharia na mafunzo ya vitendo ambayo yatafundishwa kwa lugha ya Kiswahili, ndani ya mfumo kuna video zinaonyesha hatua kwa hatua jinsi ya kusoma. Baada ya mafunzo tutatoa barua ili washiriki wapate fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo katika maeneo wanayoishi,” amesema Dkt. Shemwelekwa.

Dkt. Shemwelekwa amesema mafunzo hayo yatawawezesha wananchi waliosoma fani hizo kuongeza kipato pamoja na pato la Taifa.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Bw. Joseph Nchimbi amesema tayari walimu wa chuo hicho wamejipanga kuwafikia Watanzania watakaojisajili kupata mafunzo hayo.