Habari
TAMISEMI KUBORESHA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA, HOSPITALI YA TUMBI
TAMISEMI KUBORESHA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA, HOSPITALI YA TUMBI
Oktoba 23, 2016
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi ,Mhe. Selemani Jaffo ametoa ombi kwa Kamati ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa kusimamia na kuhakikisha changamoto zinazoikabili Shirika la Elimu Kibaha na Kurugenzi zake ikiwemo kurugenzi ya Afya ambayo ndiyo inasimamia Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.
Jaffo ametoa ombi hilo tarehe 21 Oktoba , 2016 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na Serikali za Mitaa ilipotembelea Shirika la Elimu Kibaha kuona shughuli za maendeleo na changamoto zinazoikabili Shirika hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Dickson Rweikiza amepongeza sana Shirika la Elimu Kibaha kwa kazi kubwa inayofanya alitaja maeneo ambayo Shirika limekuwa likifanya vizuri ni pamoja na uwekezaji ambapo Kampuni ya Organia tayari wamewekeza kwenye ufugaji wa kuku wa kisasa.
Aidha, Hospitali ya Tumbi imetajwa kuwa ni moja ya Hospitali bora Tanzania hususan katika kuhudumia wahanga mbalimbali wanaopata ajali za barabarani na hivyo kuokoa maisha ya watu wengi. Aliahidi kwa niaba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala kuwa changamoto za Shirika la Elimu zitafanyiwa kazi na Kamati yake.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Shirika la Elimu Kibaha ,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Dkt. Cyprian Mpemba amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya rasilimali fedha, Shirika limekuwa likijitahidi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Elimu Kibaha Profesa Patrick Makungu amesema Shirika la Elimu Kibaha kwa sasa lipo katika mabadiliko makubwa ya kiutendaji ikiwemo suala la kuongeza uwekezaji ili iwe ni chachu ya kuongeza mapato yake.
Shirika la Elimu Kibaha limeasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1963 wakati huo likiitwa Tanzania Nordic Project likiwa chini ya ufadhili wa Nchi za Nordic na lilianza rasmi tarehe 1, Januari,1970 baada ya kutangazwa katika gazeti la Serikali GN No 2 ya mwaka 1970.