Habari
TUGHE SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA WAFANIKISHA KONGAMANO LA WAFANYAKAZI

Na Lucy Semindu – :Kibaha
Vyama vya Wafanyakazi ni muhimu sana katika kuhakikisha kuwa kuna mahusiano mazuri mahala pa kazi ndio maana TUGHE Shirika la Elimu Kibaha wameandaa Kongamano kwa lengo la kuwashirikisha Vijana.
Kongamano hilo limefanyika leo katika ukumbi wa B. Merlin ambapo mgeni rasmi alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha aliyewakilishwa na Bi Chiku Wahady ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Rasilimali watu na Utumishi.
Akifungua rasmi kongamano hilo Bi Chiku Wahady amepongeza TUGHE Shirika la Elimu Kibaha kwa kuandaa Kongamano hilo kwani ni chachu ya kuboresha utendaji wa kazi. Alisistiza kwa kusema kwa kuwa washiriki wengi wa Kongamano hilo ni vijana itawawezesha kufahamu sheria mbalimbali za kazi na wajibu wa mwajiri na mtumishi mahala pa kazi
Akitoa salamu kwa washiriki wa Kongamano hilo Mwenyekti wa TUGHE Mkoa wa Pwani Bi Catherine Katele amewaeleza washiriki kuwa wakati wa sasa ni wa majadiliano mahala pa kazi ili shughuli za kila siku ziweze kufanyika kwa ufanisi mkubwa na kwamba kongamano hilo litawapa ufahamu mkubwa wa sheria za kazi.
Awali akiwatambulisha washiriki wa Kongamano hilo Mwenyekiti wa TUGHE Shirika la Elimu Kibaha Bw. Joseph Nyakyoma amesema lengo la Kongamano hilo ni kuwawezesha watumishi hasa vijana kujiunga na TUGHE, kufahamu wajibu wao wakiwa kazini na kufahamu sheria za kazi.
TUGHE ni Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Watumishi wa kada ya Afya na imekuwa ikitoa mchango mkubwa wa kuboresha haki na wajibu wa watumishi nchini Tanzania.