Habari
HOSPITALI YA TUMBI YAPATA UFADHILI WA MTAMBO WA OXYGEN.

HOSPITALI YA TUMBI YAPATA UFADHILI WA MTAMBO WA OXYGEN.
- NI WA KWANZA WA AINA YAKE NCHINI TANZANIA
Tarehe 1 Septemba ,2016
Hospital Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi yakabidhiwa mtambo wa hewa ya Oxygen uliogharimu sh. Million 184 ambao utasaidia wagonjwa wenye mahitaji wakiwemo wahanga wa ajali za barabarani .
Mtalaam wa vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, bw.Josiah Kulwa alisema mtambo huo umenunuliwa kwa ufadhili wa Serikali ya Denmark kupitia Kampuni Oxymat kwa kushirikiana na Pulse Health care na Hospital ya Tumbi.
Wafadhili hao walitoa Sh. Million 120, huku Tumbi ikichangia Sh. Million 64 zikiwa ni fedha za kusafirisha na kufunga mabomba ya kusambaza Oxygen wodini. Ambapo kufungwa kwa mtambo huo kutaokoa Sh. Million 10 ambazo zilikuwa zikitumika kila mwezi kununua gesi kutoka Tanzania Oxygen. Pia wakati mwingine nishati hiyo hukosekana na kuagizwa Nairobi, Kenya ambapo gharama huwa kubwa zaidi.
Mapema akizindua na kushukuru wafadhili wa mtambo huo ,Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema mbali na kupunguza gharama kufungwa kwa mtambo huo pia kutawapunguzia wauguzi adha ya kubeba mitungi mizito ambayo inaweza kuwaletea ulemavu pindi itakapowaangukia wakati wa ubebaji na kupunguza muda uliokuwa unatumika kuweka mitungi ya Oxygen katika wodi.
Mtambo huo pia una uwezo wa kuzalisha hewa ya Oxygen mitungi 10 ya kilo 50 kwa muda wa saa nane na gesi hiyo kupitia kwenye mitungi hiyo na kusambazwa moja kwa moja wodini. Na ina uwezo wa kusambazia wagonjwa 75 kwa wakati mmoja na pia ina uwezo wa kuzalisha gesi nyingi zaidi na kuuza katika hospitali za wilaya na zahanati.
Pia Mhe. Mhandisi Ndikilo aliomba wadau mbalimbali kusaidia kupatikana kwa kipimo cha CT Scan ambacho kitarahisisha utoaji huduma kwa wahitaji wengi ambapo mwanzo wagonjwa waliokuwa wanahitaji huduma hiyo walikuwa wakipelekwa katika hospitali ya Muhimbili.
Hospitali ya Tumbi ni Hospitali ya kwanza ya Mkoa nchini Tanzania iliyobahatika kupata mtambo wa gesi ambao ni muhimu kwa uhai wa binadamu.