Habari
VIJANA WA KIMASAI WA CHALINZE CHAMAKWEZA WAJITOKEZA KUCHANGIA DAMU KATIKA HOSPITALI YA TUMBI

VIJANA WA KIMASAI WA CHALINZE CHAMAKWEZA WAJITOKEZA KUCHANGIA DAMU KATIKA HOSPITALI YA TUMBI
NA: LUCY SEMINDU SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA
Tarehe 13 Juni,2016
Vijana wa Kitongoji cha Chamakweza Chalinze wamejitokeza kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu katika hospitali ya Tumbi. Tukio hili muhimu limefanyika ikiwa dunia inaadhimisha siku ya uchangiaji damu ambayo ni tarehe 14 Juni ya kila mwaka.
Vijana hao waliojitolea damu wamehamasishwa na Mchungaji Josephat wa Kanisa la Goshen la Chalinze Chamakweza. Mchungaji Josephat alibainisha kuwa amewahamasisha vijana hao kujitokeza na kufanya matendo ya huruma ya kuokoa maisha ya binadamu wengine kwa kuwachangia damu.
kwa upande wake kijana Gabriel Joseph baada ya kuchangia damu alisema kuwa baadhi ya Jamii ya Wamasai waishio Chamakweza walikuwa na imani potofu kuwa mtu akichangia damu hufa. Aliweza kuthibitisha kuwa jambo hilo siyo kweli kwani amechangia na damu aliyochangia itaokoa maisha ya mtu mwingine mwenye uhitaji mkubwa wa damu.
Kwa pande wake Mratibu wa damu salama katika Hospitali ya Tumbi bi.Elisia Towo amewashukuru vijana hao wa Jamii ya Kimasai kwa kujitokeza kuchangia damu. Amesema kuwa binadamu hawezi kupata damu sehemu nyingine yoyote isipokuwa kutoka kwa binadamu mwenzake na kwamba uchangiaji wa damu huokoa maisha.
Shirika la Elimu Kibaha kupitia Tumbi Hospitali inaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine.