Habari

​Wadau wa maendeleo waombwa kuchangia upanuzi Chuo cha Afya Kibaha


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Robert Shilingi leo Alhamisi tarehe 27/07/2023 amewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuliunga mkono Shirika hilo katika mradi wa upanuzi wa Chuo Cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCOHAS).

Bw. Shilingi amezungumza hayo katika mkutano na baadhi ya wadau wa maendeleo akiwataka kuunga mkono jitihada za KEC kutimiza malengo yake ya kupambana na adui maradhi, ujinga na umasikini kwa njia ya kutoa elimu.

“Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi (KCOHAS) ni moja ya taasisi zilizo ndani ya KEC, kimeanzishwa mwaka 1968 kwa lengo la kutoa elimu ya afya. Tunatakiwa tuwe na mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia hivyo tumeamua kuwashirikisha wadau wetu ili mjue mahitaji yetu na mtuunge mkono. Tunawashukuru wadau mliofika leo NBC Kibaha, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, NMB Kibaha, MEDWELL, HANWAE na KAMAL, aidha wale tuliowashirikisha na mkatoa udhuru ya kufika naamini tutaendelea kushirikiana.” amesema Bw. Shilingi.

Akiwasilisha taarifa ya chuo katika mkutano huo, Mkuu wa KCOHAS, Dkt. Tusekile Solile ameeleza kuwa mbali na changamoto za miundombinu ya madarasa waliyonayo, chuo hicho kimefakiwa kutoa wataalam wa afya zaidi ya 2000 waliohitimu chuoni hapo na hivi sasa wanafanya kazi sehemu mbalimbali.

“Kikawaida wanaoomba kujiunga na chuo chetu ni wengi ila wanaopata nafasi ni wachache kutokana na uhaba wa miundombinu ya madarasa. Mfano kwa mwaka 2021/2022 walioomba kujiunga walikuwa 3024 ila waliopata nafasi ni 157 sawa na asilimia 5.2 ya wote walioomba,” amesema Dkt. Solile.

Jumla ya Tsh. 1,205,998,114 zinahitajika ili kujenga jengo la ghorofa moja lenye madarasa mapya 5 ambapo kila moja litachukua wanafunzi 63, maabara 3, ofisi 10 kwa ajili ya wakufunzi na matundu 18 ya vyoo. Kukamilika kwake kutawezesha kuongezeka kwa idadi ya kozi zinazotolewa, kudahili wanafunzi wengi zaidi ya wanaodahiliwa sasa na kuongeza wataalam wa afya ambao wataenda kufanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini.

Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCOHAS) ni chuo cha Serikali kinachomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha (KEC), kwa sasa kinatoa kozi mbili tu ambazo ni stashahada ya uuguzi na ukunga na stashahada ya utabibu.