Habari

​Wahitimu KFDC watakiwa kutumia fursa zilizopo kwenye jamii kuonyesha ujuzi wao


Wanafunzi wahitimu Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC) jana tarehe 11/11/2021 wametakiwa kutumia fursa zilizopo kwenye jamii kuonyesha ujuzi walioupata kwenye mafunzo wanayohitimu.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu Ndugu. Gerald Mweri ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo ya wanafunzi wa mwaka wa pili.

Ndugu. Mweri amewataka wahitimu hao kwenda kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa fursa za ufundi walioupata ni nyingi. “Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fursa mbalimbali kwa jamii. Mkitengeneza vikundi kulingana na ujuzi mlioupata, nafasi za kupata mikopo isiyo na riba ipo na inatolewa na Halmashauri, nendeni mkatumie fursa hizo" Amesema Ndugu. Mweri.

"Fursa ni nyingi, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa bilioni mia tatu na nne kwenye sekta ya elimu tu kwa ajili ya kujenga madarasa elfu kumi na tano nchi nzima, mabweni kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Majengo yote yatajengwa na mafundi wa ndani na mafundi wa kawaida 'Local Fundi'. Hivyo nafasi mnayo nendeni mkaonyeshe mfano huo." Amesema Ndugu. Mweri

Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wote, Ndugu. Lucy Benedict Alloyce alimweleza mgeni rasmi kuwa mahafali hayo yanawahusisha wanafunzi wahitimu 148 kati yao wasichana ni 49 na wavulana ni 99 wanaomaliza katika fani za ufundi umeme wa majumbani, ufundi magari, ufundi bomba, ufundi uwashi, ufundi wa uundaji na uungaji wa vyuma, ushonaji na ubunifu wa mavazi, upishi na usimamizi wa hotelia, kilimo, mifugo, useremala na mafunzo ya muda mfupi katika fani za udereva, kilimo cha bustani na ufugaji wa kuku.

"Chuo kimetusaidia kwa kiasi kikubwa kupata ujuzi wa kutosha utakao tusaidia kujiajiri na kuajiriwa. Pia chuo kinatoa mafunzo kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kushiriki katika maendeleo yao binafsi, jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla." Amesema Ndugu. Lucy Alloyce.

Akisoma taarifa ya Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Mkuu wa Chuo hicho Ndg. Joseph Nchimbi alisema kuwa wahitimu hao walioanza masomo yao mwezi Januari 2020 na wanatarajia kuanza mitihani yao ya kumaliza chuo tarehe 29/11/2021 na kumaliza tarehe 10/12/2021.

Chuo cha Maendeleo ya wananchi Kibaha kipo chini ya Shirika la Elimu Kibaha na kilanzishwa mwaka 1964 kama kituo cha wakulima na baadaye kubadilishwa kuwa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.

"Chuo kinatoa mafunzo kwa nadharia na vitendo ya muda mrefu kwa miaka miwili na muda mfupi kwa miezi mitatu hadi sita isipokuwa kozi ya udereva ambayo hutolewa kwa miezi miwili tu. Pia chuo hutoa nafasi kumi (10) kila mwaka kuhudumia wanafunzi wenye ulemavu wa aina tofauti ili kujifunza aina tofauti za ujuzi wanazochagua wanafunzi wenyewe kujifunza kwa muda wa miezi sita." Alisema Ndugu Nchimbi.

Aidha ndugu Nchimbi alieleza changamoto walizonazo ambazo ni changamoto za Uchakavu wa majengo, upungufu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, upungufu wa mashine na mitambo kwenye karakana zilizopo, uchakavu wa miundombinu ya umeme, maji safi na maji taka, upungufu wa watumishi kwa baadhi ya fani, upungufu wa karakana za magari, umeme, ujenzi na useremala kwa ajili ya kufanyia mazoezi kwa vitendo.

Wakati huo huo, chuo kimetoa ombi maalum la kuomba msaada wa ukarabati wa majengo ya chuo na miundombinu yake kupitia fedha za miradi mbalimbali Serikalini.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na Mhe. Diwani wa Kata ya Tumbi Dkt. Raymond Chokala, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Ndg. Robert Shilingi, Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Shirika la Elimu Kibaha, Viongozi wa dini, watumishi wa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Wazazi na Wanafunzi wa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.