Habari

Wahitimu mafunzo ya Udereva watakiwa kupata mafunzo ya Huduma kwa Mteja


WAHITIMU MAFUNZO YA UDEREVA WATAKIWA KUPATA MAFUNZO YA HUDUMA KWA MTEJA

Na: Lucy Seminudu- Shirika la Elimu Kibaha

Tarehe 21,Juni,2016

Hayo yamesemwa na Bw. Zakharia Solomoni aliyemwakilisha  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha katika mahafali  ya 42 ya mafunzo ya Udereva ya  Chuo cha Maendeleo ya Jamii  (KFDC) yaliyofanyika leo katika Ukumbi wa Twiga wa Shirika la Elimu  Kibaha.

Aidha. Bw. Solomon aliwapongeza wahitimu wa mafunzo hayo ya udereva na aliwataka wasome mafunzo ya huduma kwa mteja kwani mafunzo hayo yatawasaidia kuhudumia vizuri wateja wao ambao ni abiria.

Pia aliwataka wawe mabalozi wazuri wa usalama barabarani na kwamba anaamini elimu waliyoipata wataitumia vizuri kwa kuendesha magari kwa usalama na kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa ni nyingi sana nchini Tanzania.

Awali akitoa historia ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha ,Mkuu wa Chuo Bi Anne Kuoko alisema Chuo hicho mwaka huu kimeweza kufanya mahafali ya 42 ya mafunzo ya Udereva ambapo wahitimu 43 wamefudhu mafunzo ya udereva.

Alifafanua kuwa chuo hicho kina kozi za mafunzo marefu na mafupi na kwamba katika kozi fupi wanatoa mafunzo ya Udereva ,Ufundi umeme,Bomba  na Mafunzo ya Ushonaji.

Kwa upande wake Bw. Angelo Nkwera akisoma risala kwa niaba ya wahitimu hao ameshukuru kwa  mafunzo mazuri waliyopata kwani yamewasaidia kupata elimu ya msingi ya udereva, elimu kwa vitendo,  kufahamu kanuni za usalama wa barabarani ,mbinu za kujihami na uendeshaji bora .

Ajali za barabarani zimekuwa ni nyingi sana nchini na Serikali kupitia Kikosi cha Usalama Barabrani imekuwa ikihimiza madereva kupata mafunzo sahihi ya udereva ili kupunguza ajali za barabarani.