Habari

​Walimu 38 watunukiwa vyeti Shirika la Elimu Kibaha


Walimu 38 wa shule zilizoko chini ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) wamepongezwa kwa kufanikisha ufaulu mzuri kwa wanafunzi waliofanya mitihani ya Taifa ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na kidato cha sita mwaka 2021.

Shule zilizoko chini ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ni Shule ya Sekondari Kibaha, Shule ya Sekondari Wasichana Kibaha, Shule ya Sekondari Tumbi na Shule ya Msingi Tumbi.

Pongezi hizo, zimetolewaJumatano tarehe 30/11/2022 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, Bw. Robert Shilingi kwa kuwapa vyeti vya kutambua juhudi zao akiwa mgeni rasmi kwenye kikao kazi cha Kurugenzi ya Huduma za Elimu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Bertil Mellin uliopo katika Shirika hilo.

Akitoa pongezi hizo, Bw. Shilingi amewataka walimu wa Shirika la Elimu Kibaha kusimamia utekelezaji wa malengo waliyojiwekea ili kuwajengea wahitimu wa shule za KEC ujuzi utakaowasaidia kujiendeleza zaidi, kujenga Taifa bora na kuleta picha nzuri ya Shirika kwa jamii.

“Sehemu kubwa yenye watumishi wengi katika Shirika letu ni Kurugenzi ya huduma za Elimu. Matokeo ya kazi nzuri mnayoendelea kufanya, ndiyo uhai wa Taasisi yetu,” alisema Bw. Shilingi.

“Nawapongeza sana kwa kuandaa kikao kazi hiki, naamini pia mtakayoyajadili na kuazimia mtayafanyia kazi,” alisema Bw. Shilingi.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma za Elimu wa Shirika la Elimu Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa amewataka walimu wote kuongeza ufanisi katika ufundishaji wao ili idadi ya masomo yenye matokeo mazuri iongezeke kitaifa.

“Utoaji huu wa tuzo za vyeti vya kuwatambua walimu hawa ambao masomo yao yalitoa matokeo mazuri kitaifa, iwe dira na motisha kwetu ili tunapoenda kutenda kazi kwa mwaka 2023 tuongeze ufanisi zaidi katika ufundishaji,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

Tuzo hizo zilitolewa kwa walimu wa masomo ya Kiswahili na Uraia darasa la nne kwa Shule ya Msingi Tumbi, Sayansi na Kiswahili darasa la saba kwa Shule ya Msingi Tumbi, Kingereza, Book keeping na Kiswahili kidato cha pili kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha, Baiolojia, Kiswahili na Kingereza kidato cha pili kwa Shule ya Sekondari Kibaha.

Pia, tuzo zimetolewa katika somo la Uraia, Kingereza na Kiswahili kidato cha pili kwa Shule ya Sekondari Tumbi, Historia kidato cha nne kwa Shule ya Sekondari Kibaha, Nutrition, Kiswahili na Kemia kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha, Baiolojia, Historia na Kiswahili kwa kidato cha nne kwa Shule ya Sekondari Tumbi; Biashara, Hesabu na Kilimo kwa kidato cha sita kwa Sekondari Kibaha.