Habari

​Wanafunzi Sweden wafanya ziara Shirika la Elimu Kibaha


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Thoren (TBS) iliyopo jijini Orebro nchini Sweden leo wakiwa na walimu wao wametembelea Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na wanafunzi wenzao wanaosoma katika shule za sekondari zilizopo chini ya Shirika hilo.

Akitambulisha ugeni huo, mratibu wa uhusiano baina ya Shirika la Elimu Kibaha na Sweden, Bw. Georges Ngonyani amesema Shirika la Elimu Kibaha limekuwa na uhusiano mzuri na shule za nchini Sweden katika nyanja mbalimbali.

“Lengo la uhusiano wa TBS na KEC ni kubadilishana uzoefu katika elimu hasa ya ujasiriamali ili vijana wanafunzi wa kitanzania waweze kupata ufahamu wa kujiajiri yaani kuibua mawazo ya kibiashara na kuyaendeleza na kuondoa fikra ya kuajiriwa pekee pindi wanapomaliza muda wao wa masomo,” amesema Bw. Ngonyani.

Katika ziara hiyo ya siku tano, wageni hao kutoka nchini Sweden kwa siku ya kwanza wamepata nafasi ya kutembelea shule za sekondari zilizopo chini ya Shirika la Elimu Kibaha ambazo ni Shule ya Sekondari Kibaha, Tumbi na Kibaha Wasichana kuona mazingira ya kujifunzia na kuzungumza na wanafunzi wa shule hizo.

Kihistoria Shirika la Elimu Kibaha lilianzishwa kama mradi wa pamoja chini ya wafadhili watano ambao ni Serikali ya Tanganyika kwa kipindi hicho na nchi nne za Kinordic zikiwemo Denmark, Norway, Finland na Sweden uliojulikana kwa jina la “Tanganyika Nordic Project” na baadaye kubadilishwa jina na kuitwa Shirika la Elimu Kibaha baada ya mradi huo kukabidhiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1970.

Hivyo, KEC kupitia kurugenzi yake ya elimu imeendelea kuwa na uhusiano mzuri na shule za Sweden zikiwemo Kvinnersta, Thoren Business School (TBS) na Karl Johan Music School ili kubadilishana uzoefu wa kitaaluma kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma ya elimu.