Habari

Wanafunzi wapya wa udereva wapokelewa Shirika la Elimu Kibaha


Shirika la Elimu Kibaha (KEC) limepokea wanafunzi wapya 35 wa mafunzo ya udereva ikiwa ni awamu ya 74 tangu kuanzishwa kwa kozi hiyo, huku wakitakiwa kuzingatia maelekezo ya walimu ili wawe madereva bora baada ya kumaliza mafunzo hayo.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC) Bw. Joseph Nchimbi, ambacho kipo chini ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) wakati akifungua mafunzo hayo.

Mkuu wa Chuo hicho amewataka wanafunzi hao kuzingatia nidhamu pamoja na taratibu za mafunzo kwa sababu nidhamu ni msingi wa fani ya udereva.

“Nawaombeni mzingatie nidhamu kwa kuwa ni msingi wa udereva, na nidhamu inaanzia kwenye mavazi. Hii itawasaidia kujifunza na kufuata sheria za usalama wa barabarani,” amesema Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Bw. Nchimbi.

Aidha amesema mafunzo hayo yatakuwa ya miezi miwili na kwamba yameanza tarehe 11/09/2023 na yatamalizika tarehe 11/011/2023.

Katika hatua nyingine, Mwalimu wa mafunzo ya Udereva wa chuo hicho, Bw. Erasmus Tibalibukwa amewataka wanafunzi hao kuwa makini wakati wa mafunzo hayo ili kuwawezesha kuzitambua kanuni za usalama wa barabarani.

Bw. Erasmus Tibalibukwa amesema katika kipindi cha miezi miwili wanafunzi wa udereva watajifunza udereva wa kujihami ili kupunguza majanga ya barabarani, kujifunza sheria za usalama wa barabarani, umuhimu wa kuwa na bima za magari na huduma ya kwanza ili dereva aweze kujisaidia wakati anapopata changamoto.

Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kinatoa mafunzo mbalimbali yakiwemo, ufundi umeme wa majumbani, ufundi bomba, ufundi magari, upishi, ufundi wa uundaji na uungaji vyuma, kilimo, ufundi uashi, ufundi seremala na ufundi wa ushonaji na ubunifu wa mavazi.