Habari

Wanawake Shirika la Elimu Kibaha watoa msaada kwa wanafunzi


Wanawake Shirika la Elimu kibaha (KEC) leo tarehe 07/03/2023 wametoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Wasichana Kibaha kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08 Machi 2023.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wafanyakazi wa KEC, Bi. Felician Mmasi amesema wameguswa kuwasaidia taulo watoto hao wa kike ili waweze kujihifadhi pale wanapopatwa na dharura hatimaye kusoma kwa utulivu.

“Wanawake wafanyakazi wa Shirika la Elimu Kibaha, tumewaletea taulo hizi za kike ziwasaidie pale mnapopata dharura, tunaziweka kwenye ofisi za walimu, mnaruhusiwa kuziomba mnapopata uhitaji ili kuwaletea utulivu wakati wa kusoma,” amesema Bi. Mmasi.

Msaada huo umeenda sambamba na kuwakatia bima ya afya watoto wawili wenye uhitaji Morisia Mchape na David Mchape na kumpatia msaada wa fedha taslimu Tsh. 324,200 mtoto Paulina Ndabile, anayeishi kwenye mazingira magumu yeye na wadogo zake wawili ambaye amemaliza kidato cha nne mwaka 2022 katika Shule ya Sekondari Tumbi na kufanikiwa kupata ufaulu wa daraja la pili.

Siku ya Wanamke Duniani huadhimishwa tarehe 08 Machi kila mwaka kwa jamii kuungana na kusheherekea pamoja huku wakitafakari fursa na changamoto zinazowakumba wanawake kwenye maeneo mbalimbali na namna ya kukabiliana nazo.

Kauli mbiu ya mwaka huu 2023 ni “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia: Chachu katika kuleta usawa wa kijinsia.”