Habari

Watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha wapatiwa mafunzo ya kutambua viashiria vya vihatarishi kwenye kazi zao.


Watumishi wawakilishi kutoka Kurugenzi na Vitengo vya Shirika la Elimu Kibaha siku ya Alhamisi tarehe 02/09/2021 wamepatiwa mafunzo ya kutambua viashiria vya vihatarishi katika maeneo yao ya kazi na namna ya kuandaa mpango wa kuondoa vihatarishi hivyo ili kuleta ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika kwa ujumla.

Akifungua mafunzo hayo, Bi. Hildegarda Saudari ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji wa Shirika la Elimu Kibaha amewataka washiriki hao kufuatilia mafunzo hayo kwa umakini ili waweze kubaini viashiria hivyo katika maeneo yao ya kazi kwa urahisi.

“Kwenye mafunzo ya leo, mtapitishwa kwenye mada mbalimbali ambazo zitawapa uelewa kuhusu kubainishe viashiria hivyo na mshauri ni kwa namna gani tunaweza kuzuia visitokee au kama vikitokea visilete madhara makubwa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi wa Shirika letu kwa ujumla.” Alisema Bi. Hildegarda.

“Katika kutengeneza mpango mkakati wa kuvikabili viashiria hivyo vya vihatarishi, nyinyi ndiyo mtakuwa mnatumiwa kuandaa mpango huo kwa niaba ya Kurugenzi na Vitengo vyenu hivyo muwe wasikivu, muelewe namna ya kufanya kazi hii ili kuleta urahisi kipindi cha utekelezaji.” Alisema Bi. Hildegarda.

Wakati wa mafunzo hayo, watumishi hao wamefundishwa maana ya vihatarishi, aina za vihatarishi, sababu za vihatarishi, namna ya kuandaa mpango wa kukabiliana na vihatarishi hivyo.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku moja na yaliendeshwa na wawezeshaji wawili Bw. Ansigar Kyejo na Bw. Damas Msaki kutoka katika Kitengo cha Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji, Shirika la Elimu Kibaha.